Kipunje: Mwamuzi anayechezesha mechi akiwa na panga, shoka Dar

image

hiyo hapoUKIMUULIZA shabiki yeyote wa
soka duniani, atakwambia kwa
sasa kuna mwamuzi mmoja tu
maarufu, Howard Webb.Sifa yake
ni kuchezesha mechi ya fainali ya
Kombe la Dunia kati ya Hispania
na Uholanzi nchini Afrika Kusini
mwaka 2010.
Pia hata mechi ngumu za Ligi Kuu
England au Ligi ya Mabingwa
Ulaya amekuwa akipangwa
kuchezesha. Sahau hilo la Webb.
Tanzania kuna mtu mmoja
anaitwa Kipunje.
Huyu jamaa anaishi sehemu moja
inaitwa Mwananyamala B, Mtaa
wa Ujiji, Kinondoni jijini Dar es
Salaam.
Unaweza ukashangaa, lakini huyo
Kipunje ndiyo mwamuzi ghali
zaidi wa mechi za mchangani
kwenye wilaya zote tatu za Dar es
Salaam ambazo ni Temeke, Ilala
na Kinondoni.
Ndiye mwamuzi pekee anayeweza
kufanya kitu ambacho hata Webb
au mwamuzi yeyote wa Fifa
hawezi kuthubutu kukifanya.
Ndiye mwamuzi wa Dar es Salaam,
ambaye ni maarufu zaidi katika
mechi za mchangani na
anayechezesha mechi yoyote
iliyoshindikana kutokana na
vurugu za mashabiki au wachezaji,
haogopi chochote ndiyo maana
thamani yake ipo juu tofauti na
wengine.
Ukikutana naye ana kwa ana
mtaani huwezi kuamini kwamba
ndiye Kipunje anayeogopwa na
wakorofi walioshindikana katika
Wilaya ya Kinondoni.
Unajua kwa nini anaogopwa? Ni
hivi, anachezesha mechi akiwa
ametinga na silaha za jadi kiunoni
ndani ya bukta yake. Silaha hizo
ni panga refu upande wa kushoto
na shoka dogo upande wa kulia.
Nani atamsogelea?
Anavyojiandaa
Anavaa jezi zake bukta, fulana,
soksi na raba kisha anafunga
kamba ya katani kiunoni halafu
anachomeka panga kushoto kwake
na shoka kulia.
Anachukua kadi zake ile ya njano
anaweka mfuko wa kushoto
kifuani kwenye fulana yake na ile
nyekundu anaichomeka kulia
ananyoosha viungo anaingia
kazini.
Kivutio chake kikubwa ni silaha
anazotinga na kujiamini ambako
kumefanya timu zote korofi hata
wahuni na mateja wanaoingia
viwanjani kuogopa kumfanyia fujo
kama wanavyofanyia waamuzi
wengine.
Ndiye mwamuzi ghali zaidi. Kwa
mechi moja hulipwa kuanzia
Sh20,000 hadi Sh50,000
kulingana na ugumu na mazingira
hatarishi kwenye mchezo husika.
Waamuzi wengine hulipwa kati ya
Sh10,000 mpaka Sh12,000
kwenye mechi hizo. Kama ukiwa
na kiasi hicho huwezi kuzungumza
na Kipunje kwani ni ndogo mno
kwake.
Mwamuzi huyo ambaye jina lake
halisi ni Issa Salum Mchinjakuku.
‘Kipunje’, anasema Mchinjakuku ni
jina la babu yake mzaa baba na ni
mwenyeji wa Pwani.
Kwa nini anaitwa Kipunje?
“Niliitwa hilo jina kwa vile tangu
nikiwa mdogo nilikuwa napenda
sana ubwabwa wa kwenye hitma,
huko pia pamenifanya kujulikana
sana. Hata nikiwa na washikaji
zangu tunashtuana ni wapi kwenye
ubwabwa tuibuke. Pitapita zetu
kwenye hiyo minuso zimenifanya
nijulikane sana. Popote pale
nakwenda ilimradi kuwe na
ubwabwa.”
Chanzo cha kutumia silaha
Kipunje ambaye alizaliwa mwaka
1980 Mwananyamala jijini Dar es
Salaam, anasema alianza kufanya
hivyo mwaka 2005 baada ya
kumshuhudia mwamuzi mwenzake
aliyemtaja kwa jina la Wema
akipigwa na mashabiki mpaka
kuzirai.
“Tukio hilo lilitokea katika Uwanja
wa CCM Mwinyijuma, Dar es
Salaam ambako mashabiki wa
timu ya Amstadam ya Tandale
walimdunda Wema hadi akazimia,
walifanya hivyo baada ya
mwamuzi huyo kukubali bao la
Mchangani FC ya Mwananyamala
ambalo halikuwa na utata
wowote.
“Niliumia sana kuona mwenzangu
anapigwa hivyo bila ya kupata
msaada wowote, tena ilikuwa
karibu kabisa na kituo cha polisi,
lakini alidundwa vibaya na hata
Polisi walipoambiwa hawakutokea
kumuokoa kwa sababu wanaujua
mtiti wa wahuni wa Tandale,”
anasema Kipunje ambaye
anajitambulisha kuwa ni
Mzaramo.
“Hali hiyo ndiyo iliyonifanya
nipate akili ya kuingia uwanjani
nikiwa na silaha, lengo likiwa ni
kujilinda ili na mimi siku moja
yasije kunikuta kama yaliyomkuta
mwenzangu na kama unavyoona
hakuna mhuni au mchezaji yeyote
mkorofi anathubutu kunipiga iwe
amekubaliana na matokeo au
anapinga wanaishia kupiga kelele
tu, lakini mimi nipo salama,”
anasema Kipunje ambaye alianza
kazi ya uamuzi wa soka mwaka
2000.
“Mwaka jana silaha hizi zilinisaidia
na pengine kama nisingekuwa
nazo siku hiyo ningekuwa sipo
duniani sasa, ningekuwa
marehemu, ilikuwa katika Uwanja
wa CCM Mwinyijuma nilipokuwa
nachezesha mechi ya nusu fainali
kati ya Shideo na Baula.
“Mashabiki wa Shideo waliingia
uwanjani kwa lengo la kunipiga
kwa sababu tu nilikubali bao
walilofunga Baula, jamaa
walikuwa wamefura ile mbaya,
niliwaacha wanisogelee kwani
walikuwa hawajui kama nina vifaa
vya kazi kiunoni.
“Walipofika na kuanza
kunisukuma nilichomoa panga na
wakashituka wakatoka nduki, hali
iliyonipa ujasiri na mimi nikaanza
kuwafukuza, lakini bahati mbaya
panga liliniponyoka na kudondoka
mbali kidogo na mimi.
“Mmoja kati ya mashabiki hao
aliliwahi na kulichukua lakini
kabla hawajakaa sawa nilichomoa
shoka langu na kuanza kuwafuata
kwa kasi ya ajabu, baada ya kuona
hivyo jamaa alilitupa panga hilo
na kutimua mbio kama vile
wamemuona mtoa roho,”
anasema mwamuzi huyo mwenye
elimu ya msingi.
“Baada ya kuhakikisha wamefika
mbali nilirudi uwanjani na
kuendelea na kazi yangu na
hakuna mtu yeyote aliyeleta tena
chokochoko hadi mechi hiyo
ilipomalizika. Kitendo hicho
kilizidi kuniongezea umaarufu
katika mitaa ya Mwananyamala,
Kinondoni, Tandale na sehemu
nyingine za Jiji la Dar es Salaam
ambako mechi zote zinazohusisha
timu zenye mashabiki wahuni,
ninakodishwa nikachezeshe
hakuna mtu yeyote anayeniletea
upuuzi, nikitoa uamuzi hakuna
anayebisha kama akipiga kelele ni
huko huko nje ya uwanja.
“Mbali na mashabiki pia hata
wachezaji na hata mateja ambao
hukusanyika viwanjani nao
wananifahamu sana na kuniogopa,
tangu wajue nina silaha
nikimwonyesha mchezaji kadi
nyekundu hutoka nje kwa roho
safi kabisa bila ya kunung’unika
kwa sababu anajua akiniletea
ujinga atakiona cha mtema kuni.
“Hizi silaha zimenifanya niwe
mwamuzi wa bei mbaya kuliko
wote Wilaya ya Kinondoni.”
Familia yake inamchukuliaje
Kipunje ni baba wa watoto
watatu; Zainabu (5), Zulfa (2) na
Nasra (1) na ni mume wa wake
wawili anaoishi nao pamoja
nyumbani kwake Mwananyamala.
Anasema kuwa familia yake haijui
kama huchezesha soka akiwa na
silaha hizo za jadi kwani
anapotoka nyumbani kwenda
kazini huzificha kwenye begi
maalumu lenye jezi na vifaa
vingine vya uamuzi.
“Wake zangu wote wananihesimu
sana na hawajui chochote juu ya
jambo hilo na hawajawahi
kuniuliza, mara nyingi
ninapokuwa naondoka nyumbani
nahakikisha hizo silaha hawazioni,
nafanya hivyo ili wasipatwe na
wasiwasi waniogope, hiyo inaweza
kusababisha mapenzi yetu
yakayumba pia sipendi watoto
wangu waone,”anasema mwamuzi
huyo, ambaye ana kadi na jezi
maalumu kwa mechi za
mchangani na zile zinazoandaliwa
na Chama cha Soka cha Kinondoni
(Kifa).
Changamoto na malengo
Anasema viongozi wa Chama cha
Soka Wilaya ya Kinondoni (Kifa)
wamekuwa wakimuonya na
kumtaka aachane na silaha hizo,
lakini yeye amekuwa akigoma kwa
vile ndiyo usalama wake
anapokuwa uwanjani kwani
mchangani hakuna usalama na
ndiko anakopatia fedha nyingi za
mkupuo.
Anasema pia staili yake ndiyo
imepandisha thamani yake na
endapo ataiacha ataporomoka na
kupotea kwa vile atakuwa hana
jipya.
“Siwezi kuacha silaha zangu iwe
katika mechi za Kifa au zile za
mchangani ambazo huandaliwa na
watu wa kawaida, nitakuwa
nahatarisha maisha yangu kwa
sababu huko mashabiki hawafai
hata kidogo wengi wanafuata fujo
si mpira.
Nimewaambia nitaachana na
silaha nitakapofanikiwa kuwa
mwamuzi wa Ligi Kuu Bara,”
anasema Kipunje ambaye anadai
ni mwamuzi wa Kifa baada ya
kufanya vizuri kwenye mafunzo ya
mwaka jana.
Lakini, Katibu Mkuu wa Chama
cha Waamuzi Wilaya ya
Kinondoni, Hussein Kalindo
anasema: “Bado hajawa
mwanachama wetu, ila alipata
mafunzo na bado majibu yake ya
mtihani hayajatoka.”
Malengo ya Kipunje
“Mungu akipenda mwezi Desemba
nitahudhuria mafunzo ya TFF
kujaribu bahati yangu ya
kuchezesha Ligi Kuu.
Nikifanikiwa kupata nafasi hiyo
naamini kuwa heshima yangu
itaongezeka pia nitaheshimu zaidi
sheria 17 za soka na nitakuwa
bora zaidi kama yule mwamuzi
Hashim Abdallah aliyechezesha
mechi ya Ligi Kuu ambayo Simba
iliitandika Yanga mabao 5-0 au
Pierluigi Collina yule Mitaliano
ambaye amewahi kuwa mwamuzi
bora wa Fifa,” anasema.
Kazi nyingine anayofanya
Ukiachana na uamuzi wa soka,
Kipunje pia ni kondakta wa
daladala inayofanya kazi ya
kusafirisha abiria kutoka
Makumbusho kwenda Kivukoni
jijini Dar es Salaam.
“Kazi hii ya ukondakta naiheshimu
sana kwani ndiyo inayonisaidia
kwa kiasi kikubwa kuendesha
maisha yangu ya kila siku na
kuifanya familia yangu iwe na
amani wakati wote japo kuna
changamoto nyingi ambazo
nakutana nazo,” anasema.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

Up ↑