Magaidi watupa silaha watoroka

image

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Kenya,
Joseph ole Lenku
MAOFISA Usalama wa nchi za
Magharibi wanahofia kuwa huenda
watekaji wengi waliokuwa wakishikilia
kituo cha biashara cha Westgate,
walitoroka muda mfupi baada ya
shambulio, kwa kutupa bunduki zao
na kujifanya wateja wa duka hilo,
imefahamika.
Mpaka sasa Polisi Kenya inashikilia
washukiwa 11 wa ugaidi, akiwamo
Mwingereza mwenye umri wa miaka
35 ambaye alikamatwa kwenye
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Jomo Kenyatta Jumatatu akijaribu
kuondoka nchini humo kwa ndege ya
Shirika la Uturuki.
Mtu huyo mzaliwa wa kitongoji
kimoja jijini Mogadishu, Somalia na
aliyepewa hati ya kusafiria ya
Uingereza Mei 2011 na kupewa
hifadhi ya kisiasa nchini Kenya,
alikamatwa na maofisa Uhamiaji
baada ya kugundulika kuwa na
jeraha usoni na mwilini. Ingawa
alikuwa na viza ya Kenya, maofisa
hao hawakuwa na kumbukumbu ya
kuingia kwake nchini humo.
Mpaka jana alikuwa akiendelea
kuhojiwa baada ya kudai kuwa
majeraha yake yalitokana na
mapigano nchini Somalia.
Mwanamke aumiza vichwa
Katika hatua nyingine, Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Kenya, Joseph
ole Lenku alisema juzi kwamba
wachunguzi walikuwa wakiendelea
kufanyia kazi taarifa kuwa mwanamke
Samantha Lewthwaite alikuwa mmoja
wa magaidi walioteka Westgate.
Alisema: “Katika taarifa zetu za awali
tulieleza kutokuwapo dalili zozote
zikionesha kuwapo gaidi mwanamke
lakini jinsi tunavyoendelea tumeanza
kusikia uwezekano huo kuwapo.”
Shaka kwamba Mwingereza huyo
yawezekana alishiriki ziliongezeka
baada ya taarifa ya gazeti la Star
jijini Nairobi kukariri manusura
wakisema kulikuwa na mwanamke
aliyekuwa akitoa amri kwa magaidi
kushambulia.
Mmoja alisema: “Mwanamke huyo
hakuwa na silaha lakini kila alipotoa
amri wanaume walifyatua silaha na
kuua.” Poorvi Jain (12), ambaye
alishuhudia mdogo wake wa kiume
mwenye umri wa miaka tisa akiuawa
aliwambia walimu wake juu ya gaidi
mmoja kuwa mwanamke mweupe,
aliyekuwa akifuatana na vijana wawili
wa kiume waliokuwa wakifyatua risasi
ovyo wakilenga watu waliokuwa
ndani ya duka hilo.
Al Shabaab ilisisitiza kwamba wageni
ndio hasa walikuwa walengwa wa
shambulio hilo na kuthibitisha kuwa
washambuliaji hao kwa makusudi
walilenga Waislamu na wasio
Waislamu.
Wanamgambo hao walilenga wasio
Waislamu na takribani wageni 18
waliuawa, wakiwamo Waingereza na
raia kutoka Ufaransa, Canada,
Uholanzi, Australia, Peru, India,
Ghana, Afrika Kusini na China.
Wamarekani watano ni miongoni
mwa majeruhi.
Lewthwaite anatafutwa akihusishwa
na kinachodaiwa ni mipango ya
kushambulia hoteli za kifahari na
migahawa nchini Kenya. Mipango ya
kushambulia hoteli za Mombasa
inasemekana kufanana kabisa na
iliyofanywa dhidi ya Westgate,
ambayo inaripotiwa kupangwa wiki
au miezi kadhaa katika ardhi ya
Somalia na Al Shabaab.
Inaaminika kwamba wapiganaji wa
kigeni wanaozungumza Kingereza
ndio walichaguliwa kwa umakini
mkubwa huku mipango ya kuhujumu
Westgate ikipangwa pia kwa
uangalifu mkubwa.
Timu ya magaidi hao iliingia nchini
kupitia mipaka ya Kenya, ambayo
mara kwa mara imekuwa ikifanyiwa
doria na askari ambao wanalipwa
mishahara duni na walinzi ambao ni
wala rushwa.
Wapiganaji wa Kisomali wanasema
hawajapata kutumia magaidi wa kike,
licha ya kuwapo hisia za kuhusika
kwa Mwingereza Lewthwaite.
Wakodi chumba dukani
Inadaiwa wapiganaji hao walikodi
duka la nguo za kike katika jengo
hilo siku moja au mbili kabla ya
shambulizi hilo, na kutumia wakati
huo kuingiza dukani humo bunduki
na risasi za kutosha.
Baadhi ya wapiganaji inasemekana
walikuwa na mavazi ya kutosha
kubadilisha na kujichanganya na raia
walikuwa na hofu wakikimbia
mashambulizi hayo.
Wakati magaidi saba wakiendelea
kushikilia mateka kadhaa ndani ya
jengo hilo, askari maalumu 20 wa
Jeshi la Kenya waliingia kukabiliana
nao huku mdunguaji mmoja
akihimili askari hao kwa saa 24 akiwa
ghorofa ya tatu kabla ya askari hao
kudhibiti jengo hilo ilipotimia saa
11.45 Jumanne.
Askari wa Kenya baada ya kuingia
ndani walizima taa na kamera za
CCTV walizokuwa wakitumia magaidi
hao na kumudu kuwapiga risasi
magaidi waliosalia. Mmoja wao
alijilipua.
Juzi usiku al Shabaab ilidai kuua
watu 50 katika shambulizi la klabu ya
usiku mjini Wajir umbali wa maili 70
kutoka jijini Nairobi. Lakini Serikali
ilisema waliouawa ni watu watatu
tu.
Apigwa risasi akiokoa mtoto
Wakati huo huo, ilifahamika juzi
kwamba baba mmoja alipigwa risasi
na magaidi hao wakati akimzuia
mtoto wa miaka minne asiuawe
katika shambulizi hilo la Westgate.
Baba huyo Simon Belcher, ambaye
alijisomesha Uingereza, alikuwa
amejificha chini ya gari na mkewe na
mtoto huyo ambaye hawakuwa na
uhusiano naye, pale majeshi ya
Kenya yalipoanza kujibu mapigo
dhidi ya wapiganaji wa al Shabaab.
Wakati magaidi hao wakikwepa
mashambulizi ya bunduki, waliwaona
watu hao na kumpiga risasi Belcher.
Risasi zilimpata begani na kifuani,
lakini kwa bahati hazikumpata
sehemu muhimu za mwili. Belcher ,
ambaye ni Mkenya anayeendesha
kampuni ya utalii, kutokea nyumbani
kwake Nairobi, amelazwa hospitalini
na mkewe akimuuguza.
Mkewe aliandika kwenye ukurasa wa
Facebook kwamba walikuwa na
bahati. Waingereza 10 Hadi juzi
idadi ya Waingereza wanaoaminika
kupoteza maisha katika shambulio
hilo ilikuwa ikitarajiwa kuongezeka
hadi 10 kutokana na makadirio
yanayotolewa na magaidi hao ya
jumla ya watu 137 kuwa ndio
waliopoteza maisha.
Sita mpaka jana ndio walikuwa
wamethibitika kufa lakini wachunguzi
wanaamini miili ya Waingereza
wengine wanne inaweza kuwa
imekwama katika kuifusi cha jengo
hilo baada ya sehemu yake
kuporomoka.
Wachunguzi wa Scotland Yard
walikuwa wa mwanzo kuingia katika
jengo hilo juzi wakitaka kutambua
Waingereza hao na magaidi. Askofu
aombea magaidi Katika hali
isiyotarajiwa, Askofu Mkuu wa
Canterbury amekumbwa na lawama
baada ya kudaiwa kuwataka waumini
wake wasisahau kuwataja watekaji
hao katika maombi yao.
Askofu Mkuu Justin Welby alitaka
Wakristo wote duniani kuombea
magaidi walioua watu wapatao 67
jijini Nairobi, Kenya. Welby
aliwaambia waumini wasisahau
kuombea watekaji hao katika maombi
yao, kwa kuwa hata yeye anaombea
pande zote; watekaji na watekwaji na
waliopoteza maisha na kujeruhiwa
na kusema kufanya hivyo
kunaendana na mafundisho ya Yesu
Kristo.
Akihojiwa na BBC juzi, Askofu Mkuu
alisema: “Kama Wakristo moja ya vitu
ambavyo tunaombea ni haki na
hususan masuala yanayohusu hasira
ambayo huibuka pale kitu kama hiki
kinapojitokeza, lakini tunatakiwa
kufanya kama alivyofanya Yesu
msalabani alipoombea waliomkosea.”
Kauli hiyo imekuja siku mbili baada
ya kuandika katika blogu yake kuwa
amewaombea magaidi hao. “Leo
naombea wote wanaoendelea
kushikiliwa na watekaji katika kituo
cha biashara Nairobi, pia familia zao
na marafiki wanaosubiri kwa hamu
kusikia mustakabali wao,” aliandika.
“Naombea pia watekaji wao, kwamba
waweze kuona na kuelewa kwamba
uadui na ghasia havitaruhusiwa
kutawala.” Askofu Mkuu Welby
aliendelea kusema kuwa waathirika
wa shambulio dhidi ya kanisa nchini
Pakistan wanapaswa kuchukuliwa
kama mashahidi wa Ukristo.
Watu wapatao 80 waliuawa katika
mashambulizi mawili katika Kanisa la
Watakatifu Wote jijini Peshawar
wakati waumini wakiondoka kwenye
Misa ya Jumapili.
Askofu Mkuu Welby ambaye
anaongoza Kanisa la Anglikana
duniani, alisema waathirika wa
mashambulizi hayo walilengwa kwa
sababu ya imani yao, na kutaka
Serikali ya Pakistan kufanya iwezalo
kulinda raia wake.
“Nadhani Wakristo wanashambuliwa
katika matukio kadhaa kwa sababu tu
ya imani yao,” alisema. “Nadhani ni
kweli kusema kwamba katika Kanisa
la Watakatifu Wote tumeshuhudia
zaidi ya mashahidi 80 katika siku
chache zilizopita. “Wameshambuliwa
kwa sababu walikuwa wakithibitisha
imani yao katika Yesu Kristo kwa
kwenda kanisani na kwamba hiyo
haiwezi kukubalika katika mazingira
yoyote kwa sababu yoyote ya tofauti
za kidini.”
Filamu ya kutisha
Vikosi vya Kenya vilisema ndani ya
jengo hilo kulionekana sawa na
‘filamu ya kutisha’ kutokana na
kutapakaa kwa damu kila mahali na
miili iliyosambaa katika sakafu.
Idadi rasmi ya Serikali ya watu
waliokufa ni 67- raia wakiwa 61 na
maofisa wa usalama sita – na Kikosi
cha Msalaba Mwekundu kina orodha
ya watu 63 ambao haijulikani waliko.
Al Shabaab inashikilia kuwa imeua
watu 137.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

Up ↑