RIPOTI YA GAZETI LA RAIA MWEMA KUHUSU KUACHIWA HURU KWA AGNES MASOGANGE NA MELISA HUKO AFRIKA KUSINI..!!

image

WATANZANIA wawili, Agnes
Gerald (Masogange) na mwenzake
Melissa Edward waliokamatwa
nchini Afrika Kusini kwa madai ya
kusafirisha kilo 150 za dawa za
kulevya wanayo nafasi kubwa ya
kuachiwa wakati wowote kuanzia
sasa, Raia Mwema limeambiwa.
Ingawa ripoti za awali zilieleza
kwamba Watanzania hao
walikuwa wamesafirisha kilo 150
za dawa aina ya Crystal
Methamphetamine zenye thamani
hiyo nchini Afrika Kusini wakati
zikisafirishwa kutoka Tanzania,
imebainika kwamba adawa
walizobeba zinafahamika kwa jina
la Ephedrine ambazo hazimo
katika kundi la dawa za kulevya.
Watanzania hao walikamatwa
nchini Afrika Kusini katika
Uwanja wa Ndege wa Oliver
Tambo jijini Johannesburg wakiwa
na dawa hizo zilizokadiriwa kuwa
na thamani ya Sh bilioni 6.8.
Hata hivyo, Ephedrine –dawa
ambayo sasa imebainika kuwa
ndiyo waliyosafirisha akina dada
hao inaangukia katika kundi la
vibashirifu (precursors) yaani
dawa ambazo malighafi yake
inaweza kutumika kutengeneza
dawa za kulevya.
“Kusema kweli nguvu ya kesi ya
akina Masogange imepungua sana
mara baada ya kubainika aina ya
dawa walizokuwa nazo.
“Kama zingekuwa ni dawa za
kulevya, mambo yangekuwa
mengine lakini kwa haya
waliyokamatwa nayo, sidhani
kama kuna kesi ngumu sana.
Nataraji watapewa dhamana
wakati wowote kutoka sasa,”
kilisema chanzo cha kuaminika
cha gazeti hili ndani ya Jeshi la
Polisi.
Masogange na mwenzake
wanashikiliwa nchini Afrika
Kusini tangu Julai, mwaka huu.
Kwa mujibu wa Sheria ya Dawa za
Kulevya ibara ya 26 (1) a na b,
dawa zinazotambulika kama za
kulevya hapa nchini ni kama vile
Cocaine, Heroin, Mandrax, Bangi,
mirungi na nyingine lakini
ephedrine haimo katika kundi la
dawa za kulevya.
Ni sheria hiyo ambayo imetamka
wazi kwamba mtu anayekamatwa
na dawa hizo zikiwa na thamani
ya zaidi ya Sh milioni 10
haruhusiwi kupewa dhamana
lakini zikipungua thamani hiyo,
anaweza kupewa dhamana.
Vyanzo vya Raia Mwema
vimebainisha kwamba kwa vile
Ephedrine si dawa za kulevya
kwa mujibu wa sheria zilizopo,
watuhumiwa hao wanaweza
kupewa dhamana.
Kwa mujibu wa mwongozo wa
wadau wa mapambano dhidi ya
Dawa ya Kulevya uliotolewa
mwaka 2011, uingizwaji na
matumizi ya dawa kama hizo
zinazofahamika kwa jina la
vibashirifu, unatawaliwa na
Mamlaka ya Chakula na Dawa
Tanzania (TFDA).
Gazeti hili lilipiga hodi katika ofisi
za TFDA jijini Dar es Salaam
ambako lilielezwa kwamba
vibashirifu huingizwa nchini kwa
utaratibu maalumu kulingana na
mahitaji ya kitaifa yaliyopo.
“Unapozungumzia vibashirifu,
unazungumzia mambo ya
kitaalamu. Nitakupa mfano, kuna
mmea unaitwa Coca. Mmea huu
unatengeneza dawa za kulevya
zinazofahamika kwa jina la
cocaine lakini ni mmea huo huo
ndiyo unatengeneza soda ya
Cocacola ambayo karibu kila mtu
anatumia.
“Mtu anaweza kutumia Ephedrine
kutibu magonjwa kama vile mafua
lakini anaweza kuitumia pia kama
dawa za kulevya. Unajua baadhi
ya dawa zilizo kwenye kundi la
dawa za kulevya zinatumika pia
hadi kwenye hospitali mbalimbali
lakini kwa shughuli na kiwango
maalumu.
“Mtu akitaka kuagiza dawa hizo
ni lazima apate kibali kutoka
kwetu. Tukizikamata kwa mtu
ambaye hana kibali
tunaziteketeza.
Hiyo ndiyo adhabu ya kwanza
lakini kama kutaonekana
kulikuwapo na nia ya uhalifu, basi
mkono wa sheria utachukua
mkondo wake, alisema mmoja wa
maofisa waandamizi wa TFDA
aliyezungumza na gazeti hili kwa
masharti ya kutotajwa jina kwa
kuwa si msemaji rasmi wa
mamlaka hiyo.
Kwa mujibu wa mtandao wa
Wikipedia, matumizi ya Ephedrine
yalianza nchini China miaka zaidi
ya 200 Kabla ya Kristo na
inapatikana sana katika mmea wa
Ma Huang ambao unatumika
kutibu magonjwa mbalimbali
katika tiba za Kichina.
Mwaka 1994, aliyekuwa nahodha
wa timu ya soka ya taifa ya
Argentina, Diego Maradona,
aliondolewa kwenye mashindano
ya Kombe la Dunia nchini
Marekani na baadaye kufungiwa
kucheza soka baada ya kukutwa
na hatia ya kutumia Ephedrine
ambayo ni miongoni mwa dawa
zilizopigwa marufuku michezoni.
Raia Mwema limekosa taarifa za
kwa nini vyombo vyote vya habari
vya Afrika Kusini viliripoti
kwamba dawa walizokutwa nazo
zilikuwa ni Methamphetamine
lakini sasa taarifa mpya zinataja
kuwa ni Ephedrine.
Hata hivyo, nyaraka tofauti
ambazo gazeti hili limezipata
zinaonyesha kwamba Ephedrine
na Methamphetamine zinafanana
kila kitu tangu kwenye muundo
wa molekyuli (chembe) zake
isipokuwa Ephedrine ina kitu
kinachoitwa Hydroxil ambacho
hakipo kwenye
Methamphetamine.
Akizungumza na gazeti hili
kuhusu taarifa hizi mpya, Mkuu
wa Kitengo cha Kudhibiti Dawa za
Kulevya, Godfrey Nzowa, alisema
anafahamu kuhusu hilo lakini wao
wanaendelea na upelelezi wao
kuhusu watu waliowatuma akina
dada hao kupeleka dawa hizo
nchini Afrika Kusini.
“Haya mambo yanafanyika
huko Afrika Kusini na sisi
hatuwezi kuingilia labda kama
wakitaka kitu kutoka kwetu.
Cha msingi kwetu ni kwamba
dawa hizo zilitoka kwetu na
wasichana wale hawana uwezo
wa kuwa na mzigo wenye
thamani ile.
Tunawatafuta wahusika na
tukipata taarifa tutawapa,”
alisema Nzowa ambaye
anatajwa kujijengea heshima
kubwa kwenye vita hii dhidi ya
dawa ya kulevya.

image

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

Up ↑